UHAMISHO wa Pauni Milioni 29 wa Kipa David De Gea kutoka Manchester United kwenda Real Madrid umekwama Dakika za mwisho baada ya Mikataba yake kutokamilika kwa wakati.
Tatizo kubwa ni kuwa Dirisha la Uhamisho huko Spain lilifungwa Jana Saa 7 za Usiku kwa Saa za Tanzania wakati lile la Uingereza Leo ndio mwisho wake, hapo Saa 2 Usiku kwa Saa zetu.
Uhamisho huu wa De Gea ulihusu Kipa huyo kwenda Real na Klabu hiyo ya Spain kuilipa Man United Pauni Milioni 29 pamoja na kumtoa Kipa wao kutoka Costa Rica, Keylor Navas, kwa Man United.
Hivi sasa kila Klabu imebaki kimya lakini ripoti kutoka huko Spain zinadai kuwa Man United ndio waliochelewesha kukamilisha Uhamisho huo kwa kutuma Mkataba uliosainiwa Dakika 1 baada ya Dirisha la Uhamisho kufungwa hapo Saa 7 na Dakika 1 Usiku.
Hata hivyo, habari toka ndani ya Man United zinadai kuwa wanayo Risiti inayoonyesha kuwa Makabrasha yote yalitumwa kwa wakati.
Ikiwa ukweli ni kuchelewa kwa Makabrasha kufika huko Spain kwa wakati basi kilichobaki ni Real kukata Rufaa kwa FIFA ambao ndio wanahusika kwa Uhamisho wa Kimataifa.
Bila hivyo David De Gea atabakia Man United kwa Msimu zaidi hadi Mkataba wake umalizike mwishoni mwa Msimu huu wa 2015/16.
No comments:
Post a Comment