Wednesday, 21 January 2015

Wafanyabiashara zaidi ya 500 kutoka masoko ya Soweto, Uhindi na Soko la Matola mjini Mbeya, jana walikusanyika kwenye Mahakama ya Mwanzo mjini hapa kusikiliza kesi ya mwenyekiti wao, Honolela Mbogela aliyekamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma za kuwazuia maofisa wa Serikali kufanya kazi zao. Tukio hilo pia lilisababisha maduka yaliyo karibu na masoko hayo kufungwa kuanzia asubuhi hadi mchana. Wakizungumza nje ya mahakama, wafanyabiashara wawili kati yao, John Katia na Jane Kapesa walisema wanaamini jiji linawaonea. Walidai kuwa chanzo cha mwenyekiti wao kufikishwa mahakamani ni mgogoro kati ya jiji na wafanyabiashara kutokana na kushindwa kuzoa takataka licha ya michango mingi kutolewa na wafanyabiashara. “Tumefika hapa kusikiliza mashtaka ya mwenyekiti. Tunajua hana kosa, siyo yeye aliyegoma kulipa michango sokoni,” alisema Kapesa. “Mshikamano huu ni kuonyesha jinsi gani ambavyo hatukubaliani na jiji wanavyowanyanyasa wafanyabiashara na kuwanyima haki zao za msingi za kufanya shughuli zao.” Kutokana na wafanyabiashara hao kujaa mahakamani, iliwalazimu polisi kuimarisha ulinzi. Sambamba na hali hiyo, Mbogela alipanda kizimbani na kusomewa mashtaka ya kuzuia watumishi wa Serikali kufanya kazi. Ilidaiwa mbele ya Hakimu Ubaswege Marthew kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Januari 10, mwaka huu katika eneo la Soko la Soweto. Anatuhumiwa kuwazuia watoza ushuru kufanya shughuli zao, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi. Mshtakiwa alikana kosa na hakimu aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi.

Tuesday, 20 January 2015

Agizo la Serikali ya Tanzania kuhusu utoaji holela wa vyeti vya kuzaliwa

Mamlaka za nchi zatakiwa kuwa makini katika utoaji wa vibali vya wageni wanaoishi nchini ili kupunguza uwezekano wa kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watu wasio na sifa. Waziri wa Kazi na Ajira Gaudensia Kabaka Sekretarieti ya ajira nchini Tanzania imezitaka mamlaka nyingine za serikali kuwa makini zinapotoa vibali vya hati ya kuishi nchini pamoja na vyeti vya kuzaliwa ili kuepusha watu wasio na sifa hususani wageni kuajiriwa serikalini. Katibu msaidizi wa sekretarieti ya ajira nchini Bw Malimi Muya ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati akiongea na hotmix ilipotaka kufahamu kuhusu tuhuma za raia wakigeni kuajiriwa serikalini. Bwana Muya ameongeza kuwa Ofisi yake inahimiza vijana walioko vyuoni na mashuleni kuchukua masomo ya sayansi na Technolojia kwakua kwa sasa fani hiyo ndiyo yenye soko kubwa la ajiri duniani.

Monday, 19 January 2015

sherehe za kuapishwa Rais wa Msumbiji JK kahudhuria

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Maputo, mji mkuu wa Mozambique, usiku wa Jumatano, Januari 14, 2015, kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Filipe Jacinto Nyusi.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewasili Maputo, mji mkuu wa Mozambique, usiku wa Jumatano, Januari 14, 2015, kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Filipe Jacinto Nyusi.
Sherehe zinafanyika Independence Square, mjini Maputo leo, Alhamisi, Januari 15, 2015. Mheshimiwa Nyusi anakuwa Rais wa nne wa Mozambique tokea uhuru wa nchi hiyo mwaka 1975.
Kiongozi mwingine mkuu wa Tanzania aliyealikwa kuhudhuria sherehe hizo ni Rais wa Tatu wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ambaye amewasili akifuatana na mkewe, Mama Anna Mkapa.

Ujumbe wa Tanzania kwenye sherehe hizo ni pamoja na Mama Salma Kikwete, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mheshimiwa Mahadhi J. Maalim, Mheshimiwa Mohamed Abood Mohamed ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Philip Mangula ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa John Magale Shibuda ambaye ni Mbunge wa CHADEMA na Mheshimiwa Halima Dendegu ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.