Wednesday, 21 January 2015

Wafanyabiashara zaidi ya 500 kutoka masoko ya Soweto, Uhindi na Soko la Matola mjini Mbeya, jana walikusanyika kwenye Mahakama ya Mwanzo mjini hapa kusikiliza kesi ya mwenyekiti wao, Honolela Mbogela aliyekamatwa wiki iliyopita kwa tuhuma za kuwazuia maofisa wa Serikali kufanya kazi zao. Tukio hilo pia lilisababisha maduka yaliyo karibu na masoko hayo kufungwa kuanzia asubuhi hadi mchana. Wakizungumza nje ya mahakama, wafanyabiashara wawili kati yao, John Katia na Jane Kapesa walisema wanaamini jiji linawaonea. Walidai kuwa chanzo cha mwenyekiti wao kufikishwa mahakamani ni mgogoro kati ya jiji na wafanyabiashara kutokana na kushindwa kuzoa takataka licha ya michango mingi kutolewa na wafanyabiashara. “Tumefika hapa kusikiliza mashtaka ya mwenyekiti. Tunajua hana kosa, siyo yeye aliyegoma kulipa michango sokoni,” alisema Kapesa. “Mshikamano huu ni kuonyesha jinsi gani ambavyo hatukubaliani na jiji wanavyowanyanyasa wafanyabiashara na kuwanyima haki zao za msingi za kufanya shughuli zao.” Kutokana na wafanyabiashara hao kujaa mahakamani, iliwalazimu polisi kuimarisha ulinzi. Sambamba na hali hiyo, Mbogela alipanda kizimbani na kusomewa mashtaka ya kuzuia watumishi wa Serikali kufanya kazi. Ilidaiwa mbele ya Hakimu Ubaswege Marthew kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Januari 10, mwaka huu katika eneo la Soko la Soweto. Anatuhumiwa kuwazuia watoza ushuru kufanya shughuli zao, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi. Mshtakiwa alikana kosa na hakimu aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi.

No comments:

Post a Comment